NO FEAR FOR THE FUTURE !

 




Jina: Yakub Nyembo
Kutoka: Tanzania

Habari zangu zaidi..
  • Nyembo jr
  • MKWINDA
  • Kenyan Pundit
  • Yakub Nyembo
  • Mija Shija Sayi
  • Ndesanjo
  • Miruko
  • Kazonta
  • Zainab Yusuph
  • Mwandani
  • MK
  • Egidio
  • Mkina
  • Mponji
  • Maarifa
  • Wakenya
  • Mtangoo
  • Akiey
  • Bangaiza
  • Magaidi
  • Bakanja
  • Mshairi
  • Mom JunkYard
  • Pambazuko
  • Uaridi
  • Beatrice Daffa
  • Twaha Omar
  • :: archives
    ::Imetengenezwa na:

    :
    : :

       Sunday, June 04, 2006  


    ·Kuwafananisha Mahakimu na “Miungu watu” ni uvivu wa kufikiri.

    ·Ni sawa na mtoto mgonjwa kumchukia tabibu kwa kumchoma sindano.

    Swali hilo funguzi lililobeba kichwa cha uchambuzi huu limetokana na kitendo cha hivi karibuni cha Rais Kikwete, kutembelea magereza matatu makubwa ya Ukonga, Segerea na Keko yote ya jijini Dar es salamu, ili iwe rahisi kujua hali halisi iliyopo katika magereza mbalimbali nchini.

    Watanzania wengi walifurahishwa na uamuzi huo wa Rais wetu kwa kuwa iliwakumbusha mambo mengi watanzania hasa kuhusu upendo kati yao bila kujali tofauti zao za hali, mali na mazingira wanayoishi kwa ujumla.

    Lakini jambo moja kubwa ilikuwa ni mshangao mkubwa aliouonesha Rais wetu kutokana na hali ya msongamano wa Mahabusu ndani ya magereza hayo, wengi wao wakiwa wamekaa muda mrefu bila kusomewa mashtaka na wengine mafaili yao kupotea.

    Kutokana na tukio hilo mitazamo ya watu ilikuwa mingi na tofauti tofauti, wapo walioona kuwa kesi zinachukua muda mrefu Mahakamani, wengine walionesha hata kushangazwa kwa watu hawa wanyonge kuwekwa magerezani, huku watu wenye kuonekana na hatia machoni pa watu na ushahidi wa kutosha kuachiwa huru tena katika mazingira ya rushwa.

    Lakini wengine walijumlisha na usumbufu unaopatikana kutokana na zuio la Mahakama “Court Injection”kwa kuwa hufifisha na kurudisha nyuma maendeleo ya watu na Taifa kwa ujumla.

    Mwana fasihi na msanii mashuhuri William Sheakspeare aliwahi kusema “Ukitaka kuongoza vizuri chinja wanasheria wote” maana utapata mwanya wa kufanya kila jambo utakalo kwa matakwa yako bila kujali sheria, lakini wakiwa hai kamwe ni vigumu kukaa kimya, na kukuangalia ufanye utakavyo.

    Mfano wa hilo ni Serikali ya Zanzibar iliwahi miaka fulani kujaribu kutumia mahakimu wasio na taaluma ya Sheria na kusababisha malalamiko mengi katika nyanja mbalimbali hususani katika medani za kisiasa.

    Pamoja na hayo, ni muhimu kuangalia Katiba kwa kuwa inatuhitaji kuangalia mfumo wa Sheria wa Madola au mfumo wa kihasimu “Common Law Legal System or Adversarial System” pamoja na umaskini au uamuzi wa Serikali wa kutatizika kuajiri wanasheria wa kutosha.

    Ili tuende pamoja katika muktadha huu ni vema kila mmoja akatumbua kuwa kwa mujibu wa Sheria Kifungu 108 cha Katiba Mahakama ina uhuru na nguvu za kurekebisha nguvu za Serikali na Bunge.

    Pia inaweza kubatilisha kifungu kilichotungwa na Bunge kwa kulinda Katiba na haki ya mtu mmoja au jamii iwapo kutatokea haja ya kufanya hivyo kwa maslahi ya Taifa na jamii husika.

    Katika mifumo ya kiutendaji Serikali huwa tayari kuwafurahisha wengi kwa gharama pengine ya maisha ya wachache, kwa mfano huwa tayari kuharibu makazi ya mtu ili tu ipite barabara itakopitiwa na wananchi wengi bila kujali manung’uniko ya mkazi wa eneo lile.

    Si hivyo tu bali huamrisha hata kuharibu kwa baadhi ya mambo ya kihistoria yanayopendwa na wachache ili kuweka miundo mbinu ya kisasa inayowafurahisha watu wengi.

    Jambo ambalo pengine ni kinyume cha Mahakama ambayo humpa mtu haki yake hata kama itasababisha kuwaumiza wengi, kwa kuwa kila mtu ana haki sawa mbele ya sheria, uhuru wa kujieleza, uhuru wa kuishi kwa mujibu wa Katiba vifungu vya 25,18,14, vya katiba yetu vinajieleza.

    Maamuzi ya kisheria kama hayo yamechukuliwa mara kadhaa na mfano halisi ni kesi mbili alizozifungua Mchungaji Mtikila dhidi ya Serikali, alitumia haki yake kisheria, na licha ya kuwa Serikali ni watu, aliweza kushinda kwa kuwa alikuwa anatafsirika kisheria kuwa yupo sawa na upande ulio dhidi yake.

    Mfumo wa sheria ya madola hapa huwa hakuna hitajiko la uwingi wa mashahidi kumuweka muhusika katika hatia au kumtoa katika hatia, suala la msingi huangaliwa dhamira yake na tendo alilodhamiria na ushahidi wa tukio.

    Iwapo ametuhumiwa kwa kuvunja mlango, na alidhamiria na kuna ushahidi wa kutosha kuwa alitenda hilo hukumu huchukuliwa, lakini kama alidhamiria na hakuna ushahidi wa kutosha licha ya kwamba alitenda, sheria haiwezi kumuweka hatiani mtu huyo.

    Huenda mtuhumiwa alikuwa hana dhamira mbaya lakini ushahidi umemuweka hatiani, Mahakama humuachia huru mtuhumiwa kwa kuwa ipo kauli mbiu ya kilatini inayotumika sana katika sheria duniani kuwapa Hamasa wanasheria kufanya kazi kwa usawa yaani (Actus non facit reum nisi mensi sit rea).

    Kauli mbiu hiyo ina maana kwamba matendo na dhamira kwa pamoja humtia mtu hatiani, lakini kama tendo ni baya na dhamira ni nzuri mtuhumiwa ataachiwa huru.

    Hii inatokana na kasumba ya mfumo huu kuwa sheria huhitaji kumuhukumu mtu kwa ushahidi usio na shaka ndani yake na usio na aina yoyote ya ghiliba (convict a person beyond reasonable doubt).

    Ni kutokana na mfumo huo suala la kumuwezesha mtu asiyeweza kusema vema kupewa fursa ya kujieleza, wale wanaoogopa mahakama na polisi nao hupatiwa mwanya wa kutosha kuizoea mahakama pia na kudadavua ukweli waujuao.

    Katika hili kuilaumu Mahakama kwa kosa la kuchelewesha kesi ni utovu wa nidhamu na ukosefu wa ustaarabu, kwa kuwa hawa Mahakimu huwa wakati mwingine kama walimu wa chekechea hususani katika kuandaa mazingira ya kesi hasa mtuhumiwa anapokuwa sugu kufuata taratibu za kisheria.

    Si vema kutoandaa mazingira ili kumpa mtu haki yake eti kwa kuwa mtuhumiwa atakuwa ndani ya mahabusu kwa kipindi kirefu, ni vigumu pia kwa kutoa hukumu kwa kesi zinazohitaji upelelezi wa kutosha tena ambao haufanywi na watumishi wa Mahakama bali Jeshi la Polisi.

    Ni kweli kwa hakika iwapo mtuhumiwa atakuwa amekaa Jela pengine kwa kipindi kirefu, halafu akakutwa hana hatia mambo mengi hususani yanayohusu maendeleo yake na Taifa kwa ujumla huharibika na ama kuanza mwanzo, lakini si Mahakama inayosababisha hilo bali muundo mbovu wa majukumu ya Serikali yetu katika muhimili huu.

    Uchunguzi huchukua muda mrefu kwa sababu kadhaa, mahudhurio ya mashahidi mahakamani kwa sababu za kuumwa, kufiwa, woga, na hata kujenga ushahidi wa uongo hupoteza muda pia.

    Askari wa upelelezi ni wachache, kesi ni nyingi, hivyo muda mwingi Hakimu huambiwa upelelezi haujakamilika, kauli ambayo hakimu hawezi kuihoji kwa kuwa haitolewi na mtumishi wa Mahakama bali muendesha mashtaka ambaye ni polisi, hivyo hujitahidi kuhimiza upelelezi kukamilishwa tu.

    Mahakimu hawalimbikizi kesi bali kesi ni nyingi sana zaidi ya mahakimu, mfano kila siku si chini ya idadi ya kesi sita hufunguliwa, lakini hakimu ana uwezo wa kusikiliza kesi tatu tena kwa kiwango cha juu sana katika ufuatiliaji ama sivyo ni kesi mbili au moja kabisa.

    Mahakama inakwamishwa na mambo mengi sana, bado mafaili hupotea na huungua kwa kuwa hakuna urutubisho unaoendana na wakati katika kuhifadhi mafaili, walau basi mafaili kutolewa katika mfumo wa kuhifadhiwa katika karatasi hizi na kuwekwa katika mtandao wa kompyuta.

    Katika uhifadhi huo mpya ambao idara nyingi sana za Serikali zimekuwa zinatumia, usumbufu wa faili kupotea na kusababisha kesi kuanza upya ungeweza kutokomezwa kwa kiwango cha juu zaidi.

    Mpaka sasa nashangazwa sana na wafatiliaji wa mambo wanapolalamika kuhusu uchelewaji wa kesi bila kutafakari kwa makini sababu zinazoweza kuifanya hali hiyo kutokea.

    Siwezi kusita kuwafananisha watu hawa na watoto wadogo wanapofanya chuki kwa muuguzi anayewachoma sindano, bila kujali kuwa sababu kubwa ya mchomaji sindano huyo ni kumpatia nafuu ama kumponesha kutoka katika maradhi yanayomsumbua.

    Rushwa ni kitu ambacho kimekuwa kikiwekwa mbele sana katika suala la kesi kuchelewa eti kuwa Mahakimu hutumia muda huo kuzibadilisha kesi kimuundo na hivyo kuharibu hukumu pia.

    Swadakta! Mimi ni muungwana nakubali hilo, lakini si kwa kiwango cha kuwadhalilisha mahakimu kwa asilimia kubwa kuhusika katika suala hilo, nakubali kwa kuwa rushwa ni adui yetu mkubwa aliyeenea kila kona katika idara zetu.

    Mahakimu si malaika, mahakimu si watakatifu na si miungu kama wanavyotengenezewa dhana na wachambuzi wa mambo ya kisiasa, kupokea ama kutoa rushwa hutendeka kwa baadhi ya Mahakimu pia kama ilivyo kwa watendaji wengine wote hapa nchini.

    Lakini ni mahakimu wachache wanaopindisha sheria kwa kutumia rushwa, na wakituhumiwa kufanya hivyo hufukuzwa kazi, kuwajibishwa na hata kupelekwa mahakamani kwa mujibu wa sheria ili haki itendeke, huku yule aliyeonewa hupewa haki yake kwa mujibu wa sheria pia.

    Licha ya hilo dhana ya kisheria inatuhitaji kuelewa kuwa Mahakama si inayotoa haki bali ni sehemu inayoonesha haki ilipo na inavyopatikana (The justice is not to be seen in court but to be seen done), na hii ndio maana ukifikiri ngazi moja ya Mahakama haikuionesha haki unakwenda katika ngazi nyingine.

    Kama ingekuwa mahakama inatoa haki, kusingekuwa na haja ya kukata rufaa kwa kuwa, kusingekuwa na haki mbadala baada ya haki ya maamuzi ya kikao cha mahakama cha awali kufanyika.

    Ni muhimu kutambua kuwa Mahakama ni kitengo nyeti sana ni sehemu ya haki ni sehemu yenye upana mkubwa kuliko ambavyo hao wanaochambua mambo hufikiria, ni zaidi ya vijiwe vya kahawa ama jamaat za mazungumzo ya kuchezea dhunha.

    Kisha baada ya kutambua hivyo sasa si nia yangu watu wasihoji muenendo wa Mahakama, mahakimu, na wanaowajibika katika vitengo vya haki nchini, lakini kabla ya kuzungumza tuanze na kuchunguza kila chembe ya tatizo husika.

    Serikali sasa ianze kuangalia umuhimu wa kutoa elimu kwa watendaji na hata wanafunzi wanaochukua sheria kujifunza mbinu za upelelezi ili wapelelezi wa kesi hizi watoke moja kwa moja katika idara za mahakama kuliko vitengo vya polisi.

    Kama itakuwa ngumu kuwasaidia ajira watoto wetu wanaochukua sheria kuwasomesha upelelezi, ili waweze kupeleleza na kuweka haki bayana katika muda stahiki basi, Jeshi la polisi liwezeshwe askari wake kwenda kusoma sheria ili wajue kuwa kuchelewesha upelelezi kwa maksudi ni kumuaharibia maisha na haki mtuhumiwa.

    Mahakama sasa ziwezeshwe kuboresha mazingira yake, ofisi bora zenye kompyuta na vifaa vingine rahisi, na vile vile Serikali iwaajiri vijana waliohitimu vema sheria ili kila mshitakiwa apewe haki ya kuwa na mwanasheria wa kumtetea hata kama hana uwezo, hilo linatendeka nchi nyingi duniani ili kulinda haki ya mtu (Legal representation).

    Naomba sasa watanzania waelewe kuwa Idara ya Mahakama haipo kwa ajili ya watuhumu tu, bali pia watuhumiwa na wanastahiki utetezi wa hali ya juu bila kufuata matakwa ya siasa, na utashi wa viongozi walio serikalini.

    Mwisho.

       [ Imeandaliwa na: nyembo @ 8:37 AM ] [ ]



       Wednesday, March 15, 2006  

    Tanzania ni upi msingi wetu katika Soka?

    HIVI karibuni tulishuhudia nchi yetu ikipata heshima ya kutembelewa na ugeni mkubwa wa wanasoka, wakiongozana na kombe la Dunia la mchezo huo, pengine ilikuwa kwa mara ya kwanza katika historia ya kombe hilo kutembelea nchi yetu.

    Katika ugeni huo kuna mengi yalisemwa na viongozi wa Serikali, Chama Kikuu cha Mchezo huo na wageni wetu hao, huku watu wengi wakichukulia suala hilo kuwa ni moja ya hamasa mpya kwa watanzania.

    Hamasa itakayosababisha wajitoe kwa dhati kufanikisha lengo la kuwafikisha katika hatua nzuri ndani ya mashindano ya Taifa hili, na nje ya mipaka yetu kwenye mashindano ya kimataifa ya mchezo huo.

    Kamwe siwezi kuamini kuwa ujio ule wa kombe la Dunia ulikuwa ni hamasa ya kuinua kiwango cha Soka nchini kwetu, nakumbuka mengi yalitendwa kuhamasisha, miaka kadhaa iliyopita wapo waliotoa hamasa ya magari kwa wachezaji, wapo waliotoa nafasi ya timu kwenda kufanya mazoezi katika nchi kubwa kisoka duniani kama Brazili.

    Lakini nimewahi kujiuliza iwapo matendo hayo yaliyokuwa na lengo la kuwahamasisha wachezaji na wadau wa mchezo huo yamewafanya watanzania wabadilike, na kuitambua Soka kama ni moja kati ya michezo mingi muhimu katika jamii.

    Hata tukikubali kuwa ujio wa kombe ni motisha, halafu kisha tujumlishe na hamasa zote zilizowahi kutolewa katika nchi yetu, tunaweza kujenga ushujaa na kusema kwa dhati kuwa watanzania wamebadilika sasa kifikra, na hivyo wanaweza kuanzisha mchakato na harakati za dhati?Je zinaweza kuwa ni chachu yetu ya kupanga mikakati ya muda mrefu na mfupi ili angalau tumudu kupeperusha bendera yetu katika medani hii barani Afrika na hata Dunia kama ilivyo katika medani zingine?

    Maswali haya yamenifanya pia nijiulize ni idadi gani ya wapenzi wa Soka wanaojua historia ya Mchezo huu, licha ya wingi wao kushinda idadi ya wapenzi wa michezo mingine kama riadha, ndondi, mpira wa kikapu, mpira wa mikono na hata mpira wa magongo.

    Wapenzi wa mchezo huu licha ya kupata hamasa kwa jitihada zote zilizowahi kuchukuliwa wameweza kudumu kwa muda mrefu katika hali moja ya utulivu usio na misingi ya kimchezo, na kama ipo basi ni ule mmoja tu usiobadilika kuendana na wakati.

    Watanzania niwajuavyo mimi ni watu mashujaa, wenye kupenda kuthubutu kila kukicha, na ambao wanaweza kudumu na fikra za kuendeleza, kuupenda, na kuunda fikra mbadala ya nini kifanyike kushinda mashindanoni na hata kuwa sehemu muhimu ya mchezo huo duniani

    Miaka michache iliyopita suala lililokuwa likizungumzwa kwa msisitizo mkubwa lilikuwa ni tatizo la uongozi wa kilichokuwa Chama cha Soka nchini FAT.

    Ambacho kiligeuzwa na kuwa kichaka cha migogoro, kiwango cha kukifanyia mabadiliko makubwa na hatimaye kuingia katika mfumo wa shirikisho lenye uongozi mpya na jina jipya la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

    Naamini kwa hakika Rais Leodger Tenga atakubaliana nami kuwa kumekuwepo na ukimya mkubwa sana katika kuwaeleza ukweli watanzania nini kinaendelea kati ya TFF na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kukuza soka hapa nchini.

    Katika kutengeneza mfumo mzuri wa kutusaidia kuwa pamoja katika muktadha mzima wa makala haya ni vema kwanza kuangalia kwa makini misingi mikuu minne ya chimbuko la soka duniani, na kujiuliza ni upi ni msingi wetu miongoni mwa misingi hiyo, ili tuweze kujua ni wapi lilipo tatizo letu.

    Na hivyo kujua Serikali na TFF wanatakiwa waanzie wapi kutoa nafasi muafaka ya kuisaidia nchi yetu katika kutueleza uhalisi wa utendaji wa suala hili, na kuwezesha ahadi zao kwetu kuhusu michezo ziwe ni za matendo ya dhati kwa kuaandaa dira ya mchezo wa soka na michezo yote kwa Taifa hili.

    Nimesema misingi, kwa kuwa ndio haswa nguzo ya uendeshaji wa shughuli za mchezo huu na hata michezo mingine, hususani tunapoangalia umuhimu wa kutengeneza programu sahihi ya maendeleo ya soka katika nchi yetu.

    Kazi ya kuinua viwango vya michezo hapa nchini sio kazi rahisi, na ni jukumu la watu wa rika zote kutengeneza mpango wa kitaifa katika kuendesha shughuli nzima ya kukuza vipaji na sio kuwashirikisha watu wachache wa Jiji la Dar es salaam au Tabora.

    Haiwezi kuwa kazi ya TFF tu, au wajumbe wake bali italazimu kushirikisha wadau toka katika ngazi zote kuanzia chini katika ngazi za mitaa, kata, wilaya, mikoa, kanda, hadi Taifa na Serikali ya Tanzania.

    Wakati huo ndio ulazima wa misingi niliyoisema awali itakapohitajika kujulikana kwa jamii, kuanzia msingi wa kwanza hadi wanne, sheria zote kumi na saba kwa mchezo wa soka na sheria zingine kwa michezo mingine iwapo itahitajika kushirikisha kwa pamoja michezo yote.

    Lakini kwa kuwa nia yangu ni kuelezea soka hapa nianze na kuelezea msingi wa kwanza wa mchezo huo ambao ni Mpira wa kipaji au vipaji, (Soccer Talents) na ndio chimbuko hasa la mchezo huu ulimwenguni, ulioanza katika karne ya kumi na mbili.

    Katika nchi kadhaa msingi huu, umekuwa unatumika sana kama dira ya Taifa katika kuinua vipaji vya vijana wao kuweza kupata ajira na kuinua uchumi wa nchi husika, kupitia mikataba ya mpira wa kulipwa, ambapo Serikali hujipatia mapato kupitia kodi na mchezaji hunufaika kwa malipo kutoka klabu inayomsajili.

    Msingi huo wa vipaji umekuwa unatumika katika nchi nyingi za Ulaya kama Ujerumani, Uingereza, Ufaransa na pia katika Afrika ya kaskazini, magharibi na katika ukanda wa nchi za kusini mwa bara la Amerika.

    Ni katika msingi huu ambapo kunapatikana vipaji vya aina tatu yaani kipaji cha kawaida (Ordinary Talent), kipaji cha kati (High Talent) na kipaji cha juu sana (Super Talents) kipaji hiki cha mwisho huwa ni nadra sana kupatikana Duniani na kwamba vipaji hivyo vinagunduliwa na walimu waliobobea katika mchezo wa soka.

    Kwa ujumla Utafiti uliofanywa na Idara kuu ya utafiti, Takwimu na Masoko nchini Uingereza mwaka 1958 hadi 1959 ambapo ilikuwa baada ya mashindano ya kombe Dunia, mashinddano yaliyofanyika nchini Sweden na Brazil kuibuka mshindi kwa mara ya kwanza ndani ya bara la Ulaya, yalionesha kuwa Afrika ndio sehemu pekee iliyo na asili ya kipaji cha juu sana yaani Super Talents.

    Ni takwimu hizi zinazowafanya watafiti kuamini kuwa wachezaji wa Brazil na wale wenye asili ya Afrika wamekuwa ni bora na hucheza mpira wenye ladha na madoido zaidi (Regular and Rhythemetical soccer) ama kwa maana nyingine huitwa mpira wa asili ya Afrika.

    Hapa naomba nieleweke kuwa Wazungu ama waarabu hawana mfumo wa mchezo huu, wao hutumia sana Mpira wa kisayansi zaidi, na waliunda mfumo huo wa kisayansi ili kuuwa mfumo wa mpira wa mwafrika katika msingi wa kwanza wa soka.

    Haswa katika kifungu cha tatu, ambacho ni Kipaji cha hali ya juu zaidi (High Talents) ambacho ni kimelea asili kilichotambaa kwa kutumia biashara ya utumwa katika maeneo kadhaa ya Ulimwengu ikiwemo Brazil.

    Ingawa muundo wao huo wa mpira wa sayansi ulikuwa na lengo tofauti kwa waafrika, lakini umewanufaisha sana waafrika kumiliki hali zote mbili yaani mfumo wa mchezo wa mpira wa kisayansi, na ule wa utamaduni wa kiafrika kwa kuongeza kiwango cha Soka (football standard from African tradition soccer and scientific football)

    Najua wengi haswa wale wanaongoza vyama vya Soka na vilabu watakubali ama kutokukubaliana na haya niyaandikayo kwa sababu wamekuwa wanaongoza vilabu na vyama vya soka kwa misingi ya maneno zaidi kuliko uhalisia wa vitendo.

    Ni wazi kuwa Msingi huu wa kwanza wa Chimbuko la soka ndio uliowaibua kina Sunday Manara, Leodger Tenga, King Abdalah Kibaden, Beya Simba, Juma Pondamali, Abeid Mziba, Fikirini Magoso, Madaraka Suleimani, Suleimani Matola na wengine wengi ambao waliwahi kuwa mashujaa na wanaondelea kuwa mashujaa katika soka.

    Sina hakika mpaka sasa kama Tanzania kuna wachezaji wanaofikia hamsini waliopitia katika msingi tofauti na huu katika kukua kisoka, lakini nina hakika kuwa wengi nisioweza kuwahesabu toka miaka ya Hamsini hadi sasa wametokana na aina hii ya chimbuko katika sehemu kubwa ya nchi yetu.

    Lakini niseme kuwa vipaji hivi vimekuwa vikiishia katika sehemu ngumu mno kwa wale waliowahi kuwa wachezaji, wengi ni masikini wa kutupwa, ni ombaomba waliokosa nafasi katika jamii ya wanasoka wa ulimwengu huu.

    Nasema haya kwa uchungu mkubwa, ukimuona Beya Simba kule Mwanza, Wasitara Baribari kule Kigoma, Godwin Aswile na Suleimani Mathew kule Mbeya, hali za maisha yao ni ni tofauti na hadhi yao katika historia ya soka. Ama aliyokuwa akiishi kipa maarufu marehemu Athuman Mambosasa, hutofikiri kamwe kuendelea kucheza mpira ingawa pengine ni kipaji chako.

    Je, Taifa limewatunza vipi, limekuwa na mpango upi katika kuangalia mustakbali wa wazee hawa ambao ni hazina yetu, haiwezekani wote wapate madaraka ya uongozi wa soka lakini mchango wao ni mkubwa kuliko pengine kuongoza hilo Shirikisho la Soka, TFF imewaangalia vipi hawa wataalamu?

    Hivi karibuni Eric Cantona, mchezaji wa zamani wa Manchester United ya Uingereza, alitoa kauli yake kuwathibitishia wapenzi wa timu hiyo kuwa kuna mabadiliko makubwa kisoka kiasi cha kutoridhisha na kupoteza uelekeo.

    Cantona yupo, si mchezaji tena wa soka lakini kauli yake bado ni mapambano ya kishujaa kwa kuwa katunzwa, hawezi kukaa kimya anapoona mambo yanaharibika, lazima atumie nafasi yake ya kukumbuka faida ya kile kilichomfanya apate maisha mazuri.

    Hivi soka itakuwa vipi iwapo hakuna watu wanaopewa nafasi ya kutunza vyanzo na misingi ya vipaji ili kutoa mwanya wa muendelezo wa fikra thabiti kuwa mchezo wa mpira ni sehemu ya vyanzo muhimu vya kipato na uchumi wa nchi yetu.

    Hebu tuangalie hiki kizazi kipya ambacho pia kinatokana na Msingi huu wa chimbuko la soka nchini, wengi wameangukia katika biashara ya mitumba, chipsi, madawa ya kulevya, uporaji, na kadhalika.

    Ukienda mtaa wa Kongo, eneo la Mchikichini na hata Tazara wapo vijana wengi sana ambao waliwahi kucheza mpira kisha wakageuka na kuuacha, kwa kuwa hakuna jipya katika mfumo wa maisha ya mbele ya huyo muhusika aliyekuwa akiucheza.

    Muulize Juma Kaseja, Suleimani Matola, Boniphace Pawasa, Akilimali Yahya, wako wapi wenzao kina Mbayo Shabani, Nizari Kitumba, Mteba Mussa na wengineo, kama hawajajibu hawajui basi watasema wapo mtaa wa Kongo ama ukamuulize Kipingu?

    Hili ni tatizo kubwa, vipaji tunavyo, lakini muendelezo udumishaji, makuzi na utunzaji wa vipaji hivyo hatuna, tumeshindwa walau kuheshimu na kuenzi juhudi kubwa za wachezaji wachache tu waliojaribu kuonesha kuwa nchi yetu ni miongoni mwa nchi zenye hazina ya vipaji katika soka.

    Hebu tuangalie Msingi wa pili wa Chimbuko la soka Ulimwenguni ambao ni Mchezo wa mpira utokanao na Upandikizi, (Planting Football), ambao pia kumekuwepo na nchi nyingi zinazotumia mbinu hizi ikiwemo Mali, Nigeria, Misri na nchi nyinginezo.

    Niseme Katika msingi huu hutumika zaidi mfumo wa Programu za mafunzo kuanzia chekechea hadi Elimu ya juu, ambapo huchukua hatua sita ya makuzi ya Elimu ya kawaida ya mpandikizwa ama mchezaji mtarajiwa.

    Katika msingi huu Programu huanzia katika shule za ukuzi (Nursery soccer Development Programme) hii ni kwa watoto wa miaka mitatu na kuendelea hadi kufikia umri wa kuingia katika hatua nyingine ambayo ni hatua ya kujenga uimara (Primary Soccer Development Programme).

    Baada ya hapo vijana hawa tayari wanakuwa wapo katika maisha ya soka, soka ni rutubisho la maisha yao ya baadae, ni tegemeo lao, ni muhimu kuendelezwa na kuingia katika hatua ya sekondari (Secondary Soccer Development Programme) kisha hatua ya elimu ya sekondari ya juu (High School Soccer Development Programme).

    Hapo hatua inayofuata ni Taifa kupata wataalamu wa soka, katika hatua ya Vyuo Vikuu na Taasisi za elimu na utaalamu yaani (University and Institution Soccer Development Programme) huko ndiko wanapopatikana wataalamu kama ilivyo fani ya Usanii ama udaktari.

    Na hatua ya mwisho ni ile ya Vilabu vya kawaida (General Soccer Development Programme), hatua hii inahusu wale ambao hawakufanya vizuri katika mashule, lakini ni wabunifu na wana uwezo wa kubadilika.

    Lakini hatua hii pia hutumika kuwaaandaa vijana wenye vipaji vya aina zote tatu kama nilivyoviainisha hapo awali, kwa aina zote za misingi niliyokwisha kutaja na ile ambayo sijaitaja.

    Sehemu nyingi duniani huiita ni Programu ya vilabuni na timu za Taifa, kwa kuwa hutumika pia kuchuja na kutofautisha pamoja na kufananisha vipaji vya wachezaji waliopo, na machimbuko yao.

    Tofauti sana na hatua zingine katika msingi huu, hatua hii huwa ngumu kufikia mafanikio kwa kuwa hulazimu wachezaji kukaa kwa muda mrefu pamoja na kupewa mafunzo ili wakafanye vizuri katika mashindano.

    Ni hatua hii ambayo hutumika sana hapa nchini kama kigezo cha timu kushinda ama kushindwa kwa kuwa watu waliopo wengi hawakupitia katika hatua zingine ila hii ya sita ya kwenda kambini, lakini visivyo, kwa kuwa hukaa muda mfupi tu kama wiki tatu badala ya muda mrefu.

    Sio rahisi kutokushindwa kama tunacheza na timu kutoka katika nchi zenye kujali mfumo wa Programu hizi, labda kwa mashindano ya ndani ambayo sio rahisi kutofautisha chochote kati ya uozo wa timu moja na nyingine.

    Katika hatua zote hizi ni muhimu Taifa kuelewa umuhimu wa mafunzo ayapatayo mwanafunzi kuwa hayana tofauti na mtu anaekwenda shule za kawaida na wote wana thamani sawa mbele ya macho ya jamii na wote ni muhimu kwa Taifa.

    Ninapoandika haya leo, najiuliza hapa katika nchi yetu hakuna watu wenye kujua mambo zaidi ya haya katika soka, na kama wapo kwa nini hawasemi kwa dhati ya mioyo yao ili tubadilike?

    Kwa nini tufurahi kujengewa Viwanja na kupanga kuongeza vingine ikiwa hatuna mipango madhubuti ya kupata uongozi bora wa michezo, mbinu bora za kuzalisha wachezaji, utunzaji wa maisha ya wanamichezo, ukuzaji wa uchumi na thamani katika michezo?

    Nashindwa kuelewa kwa nini Serikali iwe mbele kutoa ushirikiano wa kutafuta fedha kujenga viwanja, huku ikiwa imefumbia macho kabisa suala lakurudisha Programu ya sita ya maendeleo ya soka ambayo iliachwa mwaka 1972?

    Programu ile iliandaa wataalamu wengi sana tena wa fani zote katika soka kuanzia walimu, watawala, waamuzi, watafiti, watu wa masoko, na sehemu zingine muhimu katika masuala ya Michezo.

    Serikali ilifanya kazi ya kuwaandaa watu kama Sylesaid Mziray, John Mwimbe, John Sapi John, Joel Bendera, Dastan Daffa, Abdulrahmani Wengi, John Sikupizi, John Elisafi na wengine wengi tu, ambao leo hii bila wao sijui tungekuwa tunakopa wapi ufundi kwa vijana wa sasa katika soka.

    Hapa najiuliza pia kuwa nini kilisababisha Programu hii ifutwe na kwa nini isirudishwe kwa kasi, nguvu na ari mpya na mifumo mipya inayoweza kukidhi hali halisi ya wakati huu.

    Kwa maana sasa wengi niliowataja wamekuwa Marehemu, wengine ni wazee hawawezi kukidhi mahitaji ya wakati huu lakini wengine sio tu ni wazee lakini wamestaafu na hata kuikimbia Wizara ile ya Kazi pale kwa jinsi ilivyojaa ubabaishaji na porojo.

    Sasa tuendelee na Msingi wa tatu wa Chimbuko la Mchezo huu ambalo hutokana na vipaji vya kuambukiza (Transimissional Football/ transimission of Talents), msingi huu hasa hupatikana mara nyingi katika pande za mipakani mwa nchi na kuletwa na wakimbizi, wafanyabiashara, watafiti na kadhalika.

    Mfano wa nchi zilizo ndani ya msingi wa Chimbuko ni Zambia ambapo wamepata maambukizo ya kisoka toka kwa majirani zao wa Kongo, ambapo licha ya Zambia kuwa na wachezaji wa vipaji tofauti, wengi lakini wanatoka kaskazini mwa nchi hiyo.

    Maeneo ya Lwanshire, Nchonga, Mfulira, na Kitwe ndio yanayoongoza kwa kutoa wachezaji wengi wa soka katika nchi ile ya Zambia maeneo ambayo hayako mbali na mipaka ya nchi hiyo na Kongo ukiangalia ramani.

    Lakini pia Tanzania tuna baadhi ya maeneo yanayopata athari za Chimbuko hili, kwa mfano Mkoa wa Kigoma, wanaambukizwa na Nchi ya Burundi, Mtwara wanapata maambukizi ya kisoka toka Msumbiji nchi ambayo ni maarufu kwa vipaji vya asili katika soka.

    Msingi huu husaidia sana kuondoa upinzani mkali kati ya nchi na nchi kwa kuwa wachezaji wa pande zote wanakuwa na uwiano wa kiutendaji kwa viwango vinavyofanana ama kutofautiana.

    Ni msingi huu unaondelea kuisaidia nchi yetu kwa kiwango cha juu sana, licha ya kuwa sehemu kubwa ya nchi yetu ina mpira wa asili hususani katika mikoa ya Morogoro, Tabora, Rukwa, Mwanza, Tanga na kadhalika.


    Hivi karibuni Msemaji wa TFF, Bw. Florian Kaijage aliutanabaisha umma wa watanzania kama si waafrika kuwa itakuwa ni vigumu kwa Timu yetu ya Taifa kwenda kucheza katika Fainali za Afrika zitakazochezwa Ghana Mwaka 2008, kauli ambayo imepingwa vikali na Rais wa Jamhuri Bw. Jakaya Kikwete.

    Bw. Kikwete alisema kuwa kauli ya Kaijage ni ashirio kuwa hakuna maandalizi ya dhati kushiriki katika mashindano hayo,jambo ambalo lina ukweli wa dhati ambapo Bw. Tenga na uongozi wake wapo mbioni kumpata Katibu mpya badala ya Bw Asher Gasabile ambaye alikuwa ni katibu mkuu wa TFF.

    Bw.Gasabile analalamika kuwa kulikuwa na mizengwe mingi ambayo imemfanya aende mahakamani kwa kutafuta haki na usawa wa dhati, jambo ambalo Bw.Tenga haonekani kulipenda sana na halimvutii na hivyo jana tu ameamua kutangaza rasmi nafasi hiyo ili isiwezekani kwa Gasabile kurudi.

       [ Imeandaliwa na: nyembo @ 6:28 AM ] [ ]



       Tuesday, March 07, 2006  

    MMEM na MMES Tumeona sasa vipi kama tukiwa na MMEVU?

    Assalamu waungwana!
    Kama twaweza tumuulize Jakaya swali hili, kwa kuwa tuliwahi kumpongeza sana katika ushindi wake nami
    nalifurahi kwa dhati kuwa miongoni mwa waliotoa pongezi kwa Rais wa awamu ya nne Jakaya Kikwete, baada ya awamu ya tatu kufikia tamati yake katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Desemba 14 mwaka jana, ulioruhusu awamu mpya kushika hatamu.

    Sote pia tulishuhudia mwaka 2002 Serikali ya awamu ya tatu chini ya uongozi wake Rais Benjamin Mkapa ikianzisha Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi MMEM na ule Maendeleo kwa shule za Sekondari MMES.

    Katika utekelezaji wa mpango huu kumeonekana mafanikio makubwa kama ujenzi wa vyumba vya madarasa, nyumba za walimu, madawati na vyoo.

    Lakini licha ya mafanikio haya kumekuwepo mapungufu pia kwa mfano kama kuna madarasa yamejengwa lakini hakuna vitabu vya kutosha au kuna nyumba za walimu nyingi lakini mwalimu aliyejengewa, pato lake linakatisha tamaa, ni mapungufu ya wazi ya mpango huu.

    Nimekuwa nikisubiri baada ya Shirika lisilo la kiserikali la Haki Elimu kukaripiwa na kuhitajika kufungiwa kwa sababu ya kutaja ama kuonesha mapungufu ya Mipango hii, iwapo Serikali itasema yenyewe, mafanikio na upungufu wa MMEM au MMES.

    Subira yangu imefika ukomo baada ya kusikia na kuona kinara wa Mpango huo Rais Mstaafu wa awamu ya tatu Benjamin Mkapa akielezea mafanikio mpaka kuondoka kwake madarakani bila kujali kuwa wananchi wanapenda kujua mapungufu.

    Mkapa kaondoka madarakani takribani miezi miwili iliyopita huku MMEM ikibakiza muda mchache tu wa kufika tamati wengi tunajiuliza iwapo itaanzishwa nyingine kwa lengo la kuboresha huduma za Afya kwa wanafunzi, walimu, kusaidia walemavu wa akili, wazee wasiojiweza na vijana waishio katika Mazingira magumu.

    Wakati ni ukuta, naam awamu ya MMEM inakwisha 2006, tumeona tuliyoyaona, pengine yataendelezwa lakini si kwa hali hii iliyopo, isiyojali Mshahara wa Mwalimu kulingana na kazi yake.

    Sidhani na sifikiri kama tutaendelea kukumbuka faida za MMEM iwapo hali haitobadilishwa na walimu kuboreshewa maisha yao, nasema sidhani!

    Kuboresha hali za walimu tu hakutoshi, ni wajibu wa Serikali mpya pia kuhakikisha njia za kuwapata walimu hawa zinakuwa bora zaidi ili kupata elimu bora na si bora elimu.

    Nasema hivyo kwa kuwa wengi wa walimu wa sasa wapo katika makundi matatu na, kundi la kwanza ni wale walimu waliopatikana katika mipango kama hii ya kuboresha Elimu ya awamu ya kwanza na ya pili Serikali zilizopita.

    Hawa ni walimu waliopatikana katika Mpango wa UPE, ambao kwa sasa wapo katika mpango wa Mafunzo ya Walimu Kazini Daraja la III B/C-A Monduli, hawa wangeweza kupatiwa ujuzi ziada katika vyuo vya Ufundi ili kufanikisha na kuhakikisha Elimu kwa vitendo katika shule za msingi inaimarika.

    Kundi la pili ni lile la walimu ambao hawakuingia kwa wito kazini bali hali ya maisha imewasukuma kuingia huko ili walau kile kidogo kinachopatikana huko kiwasaidie.

    Hawa ni wengi zaidi kuliko hata wale wa UPE waliotufundisha Sayansi Kimu, ni hatari kwa kizazi cha watanzania katika elimu kwa kuwa Lengo ni mshahara si kazi husika, ni jukumu la Serikali kuandaa mazingira ya walimu hawa kuikubali kazi yao hiyo.

    Na kama si hivyo, kuwatafutia njia mbadala ya maisha ili kuiokoa Elimu kwa mafanikio ya Taifa hili, na kuwapata walimu hawa ni kuanza kukagua utendaji wa kazi mashuleni, mahudhurio yao kazini, mahusiano yao kikazi na wanafunzi, pamoja na nidhamu yao kwa kazi zao za kila siku.

    Lakini kundi la tatu ni lile la walimu wanaotokana na wito wao katika kazi, hawa toka walipokuwa wanafunzi walitamani kuifanya kazi yao kwa sababu tofauti walizokuwa nazo, kwa bahati mbaya hawa ni wachache zaidi.

    Licha ya Uchache wao wanapatikana katika kila kona ya nchi hii, hawa ni hazina isiyomithilika ambayo inahitaji kuenziwa kwa dhati na ni muhimu kuboresha maisha yao binafsi na kuweka mazingira rahisi katika kazi yao.

    Hawa ndio wanaoifanya MMEM, kutajwa mafanikio yake kwa kiwango cha juu zaidi katika Matokeo yaliyokuwa yakisemwa na Rais aliyemaliza muda wake katika hotuba zake Bungeni na katika Mikutano yake ama katika utaratibu wake aliokuwa nao wa kuhutubia Taifa kila mwisho wa mwezi.

    Lakini bado najiuliza kulikuwa na maana gani kusifia mafaniko ya utendaji huu wa MMEM wa MMES huku hakuna mkakati maalumu wa kuwaendeleza vijana wanaomaliza Elimu ya msingi na Sekondari?

    Baada ya matokeo ya mwaka huu hali imekuwa ni ya kushtusha zaidi, wanafunzi wamefanya vizuri sana, lakini hawana nafasi ya kuendelea na masomo, si shule za msingi au kidato cha nne na sita hali imekuwa tafrani, najiuliza hawa wanakwenda mtaani au wapi na kufanya nini katika nchi maskini kama hii?

    Kwa mfano matokeo ya darasa la saba mwaka huu kwa mkoa wa Tabora yameonyesha kuwa wanafunzi 5,843 kati ya 8,8809 waliofaulu wamekosa nafasi ya kujiunga na Elimu ya Sekondari katika shule 49 za mkoa huo, Mwanza wahitimu 10,844, na Bukoba 6,951, ukijumlisha na idadi ya wale ambao hawakupata alama za kuridhisha kuendelea na masomo katika maeneo hayo, unatengeneza Taifa la Mchanganyiko tata wa ujinga.

    Mafanikio ya MMEM na MMES yanakosa nafasi kwa kuwa hayana muendelezo makini, hakuna Mpango wa kuanzisha na kuimarisha Shule mpya za Sekondari, Vyuo vya Ufundi stadi, upanuzi na uongezaji wa Vyuo Vikuu vya kutosha na vile vilivyopo kuna migomo na matatizo lukuki, lakini pia Vyuo vya michezo na utamaduni, vinavyomilikiwa na Serikali imekuwa ni ndoto.

    MMEM na MMES, juhudi za wazazi pamoja na ari ya mwanafunzi vyote vinakufa kifo kimoja, baada ya matokeo ya shule ya msingi tu kutoka, hili ni tatizo kubwa kuliko inavyoweza kufikirika.

    Kifo chenyewe kinakuja kwa kuwa hakuna Tathimini ya wazi kutoka kwa wadau wote wa elimu kuhusu mafanikio na mapungufu na nini kifanyike ili kuwasaidia waliosaidiwa na MMEM kuendelea mbele kielimu na kufikia katika kilele cha mafanikio.

    Kwa hakika haya yangefanyika na kuwekwa wazi, mafanikio yangetumika kama mifano na upungufu kama changamoto ya uboreshaji na utatuzi wa muendelezo wa Elimu kwa wahitimu wa ngazi mbalimbali za kielimu hapa nchini.

    Naamini kuwa wazazi wangependa zaidi kuona watoto wanaomaliza Shule za msingi wanapangiwa kwenda kusoma Sekondari ama kujifunza Vyuo vya ufundi kisha wakaendelea ama kukutana tena katika Vyuo vikuu kila mmoja kwa taaluma yake huku wale ambao hawatojaaliwa kuendelea kwa matatizo yao binafsi wanapata fursa safi ya kujiajiri.

    Katika hili ni muhimu kumkumbusha Rais Kikwete kuangalia kwa makini mfumo mzima wa MMEM na njia muhimu ya kuuendeleza uhai mbadala baada ya muda wake kuisha, kwa kuwa Elimu kwa shule ya msingi ni muhimu na ni kitu kinachoendelea.

    Ni kwa sababu hiyo itakayomfanya ageuze jicho lake upande wa pili na kuhakikisha Mipango madhubuti kama ulivyo wa MMEM na MMES, inawekwa kwa kuanzisha Vyuo vya Ufundi na ongezeko la Vyuo Vikuu ili kuweka mtiririko imara wa kazi ya Mipango aliyoianzisha Rais Benjamin Mkapa.

    Nimepata uwezo wa kuandika Makala hii nikimkumbusha Rais Kikwete aangalie kwa jicho lake upande huu wa vyuo vikuu kwa kuwa nakumbuka kazi za Ubunifu wake katika uendeshaji wa Wizara mbalimbali alizowahi kufanya kazi kama Waziri.

    Ingawa naona bado kuna kosa kwa kumpa walau Wizara Bw. Mungai, huyu ndie aliyeichanganya na kuikoroga wizara ya Elimu zama za Mkapa, huyu hakukuwa na haja ya kumpa Kilimo.

    Kwanza hajui kuwajibika anapokuwa ametenda kinyume, hana tofauti na Mkapa pale anapotenda kosa hupenda asikosolewe bali apewe nafasi ya kusikilizwa na kisha awashukuru kwa kumsikiliza.

    Huyu ndie aliyeanzisha sakata la Haki Elimu na nina tumai kuwa hata ikitokea kuundwa kwa haki kilimo basi atakuwa mmojawapo watakao kuwa vinara kukosoa haki kilimo hiyo.

    Nimepata pia mtikisiko na mshtuko mkubwa kwa Mh.Maggy Sita kuwa Waziri wa hiyo Elimu, huyu kwanza aliingia kwa njia haramu kabisa kisha akaishi kiuharamu, yaani kinyume cha uhalali.

    Sasa nafasi yake inatokana na walimu, huyu ni msemaji wa walimu na mtetezi aliyetarajiwa ingawa kwa upande wa wafanyakazi bado ni mtetezi haramu ambaye kama angeendelea kuwa Mbunge wa kiti cha uteuzi basi pengine angetetea kiuhalali, lakini sasa ndio basi!

    Ndio basi kwa kuwa sina shaka kuwa Waziri kazi yake sio ngeni kwetu sote, muda wote ni kuifanyia utetezi Serikali tu, hata kama haitojali haki na usawa kwa maendeleo ya Elimu kwa wananchi wake.

    Nasema hata hao walimu sasa hawana pa kushika kwa kuwa mtu wao sasa amekuwa mtetezi wa Serikali kwa kuwa aliapa kuwa yeye Magreth Sitta atailinda na kuitetea katiba ya nchi, kulinda siri ya baraza la Mawaziri na kumsaidia Rais na sio utetezi kwa walimu wetu hawa wa huko Kinampanda.

    Naomba sasa ninene kuwa simkosoi JK kwa uteuzi wake bali naonesha mtazamo wangu katika uteuzi wake, na kwa kuwa namjua kuwa sio mtu wa kudharau kauli za watu hususani wanaotumia kalamu, kama waliomtangulia waliokuwa wakikosolewa hudai anaonewa wivu.

    Naona niondoke nirudi kijijini kwangu nikasubiri iwapo kutajengwa chuo huko katika mpango wa (MMEVU) Mpango wa Maendeleo kwa Vyuo vya Ufundi, kama utaundwa lakini pia nawaalika waungwana wanaofuatilia mabadiliko ya Soka la Tanzania kutokukosa kufuatilia mfululizo wa makala zangu kuhusu misingi ya Soka la Tanzania na matatizo yake ambazo nitaanza kuzitoa wiki ijayo.

    Wakattabahu!

       [ Imeandaliwa na: nyembo @ 2:04 AM ] [ ]



       Wednesday, January 25, 2006  

    Bw.Makene naona amesahau kuwa mtu mzima hatishiwi "Nyau" kaandika katika Tandopepe lake Shairi la kunitisha chungulia!, nami kwa kuwa nina asili ya Ushujaa, mtu nisiye lelemama hasa katika kila jambo lenye kuonesha maarifa na ukamili wa utendaji nimeona nimjibu. kwa kuwa mimi ni Muungwana naweza anza kumsalimu hapa kwa kumueleza kwa ufupi kasoro zake na kumueleza kuwa mimi si teketeke kama mwanzo nimekomaa

    "heshima ataijenga, hoja kuzipangilia,
    atakoma tongatonga,tungo atanitungia,
    sio sifa kuzipanga, Ubush kuringishia.
    naja hiwa' mekomaa,kuzidi nilivyo mwando".



    'SISEME SIKUKWAMBIA, WAJIPALIA MAKAA.

    Nakuzerwa wajiwasha, wajisifu kama ndovu,
    Utungo ‘mekulewesha, huutambui uovu,
    Je,ngomayo yakesha, au ni nguvu ya povu?
    ‘siseme sikukwambiya, wajipalia makaa.


    Wewe ni rafiki yangu, nia nilokuswafiya,
    Wewe kama ndugu yangu, tulo zaliwa pamoya,
    Huwa napata utungu, wembe unapoliliya,
    ‘siseme sikukwambia, wajipalia makaa.

    Ninenayo zingatiya, uache wako uchizi,
    Hata ukijisiya, mimi si yako saizi,
    Mwisho utakujaliya, tena ya damu matozi,
    ‘siseme sikukwambiya, wajipalia makaa.

    Wajivundiya heshima, kwato hito kiburicho,
    Wapenda sana lalama, kwa kila nikuambiacho,
    Ungenda enga nyuma, ujuwe kikufatacho
    ‘siseme sikukwambiya,wajipalia makaa.

    Najua raha waona, kwa utunzi utungao,
    Fahamu’mekuwa huna, imekupotea kwayo,
    Hata watu wangenena, wewe hutojali hayo,
    ‘siseme sikukwambia, wajipalia makaa.

    Asali nayo ni tamu, ambayo umenyonyeya,
    Ndani yake mna sumu, kama hujui sikiya,
    Utakuja jilaumu, muda ‘takapo wadia
    ‘siseme sikukwambia, wajipalia makaa.

    Kipofu ‘megeuka, umepofuka matoni,
    mtu japo angataka,kukuonesha huoni,
    mkono angakushika,kamwe hutoutakani,
    ‘siseme sikukwambia, wajipalia makaa.

    Pole, ninakutakia, Nakuzerwa haramia,
    Kitambo nalikwambia, kwa nini umeamua,
    Kwa Bush kwenda lowea,tabia kuharibia,
    ‘siseme sikukwambia, wajipalia makaa.

    Ghaibuni jisifia, bila soni watungia,
    Marekani tumikia, utumwa unopendea,
    Sisi wana Tanzania,nchi yetu twasifia,
    ‘siseme sikukwambia, wajipalia makaa.

    Madharani ‘tangia, ujipalie makaa,
    Watu wataangalia,ukweli nakuambia,
    Kama hutojitunzia, ukawata mbovu ndia,
    ‘siseme sikukwambia, wajipalia makaa.

    Siseme sikukwambia, rafiki yangu muhibu,
    Kwa kusudi ninasema, huna la ziada kwangu,
    Kusudi ni kukuponya, nakuambia mwenzangu,
    ‘siseme sikukwambia, wajipalia makaa.

    Wewe tena si mtoto, eti nitakukemeya,
    Wala kushika ufito, makalio kuchapiya,
    Kwangu haya ni mazito, siwezi kukutendeya,
    ‘siseme sikukwambia, wajipalia makaa.

    Kaditama ukisiti, hili liwaze sikome,
    Moyoni uyadhibiti, akilini uyapime,
    Kidume mwando hayuti,mayuto huya kinyume,
    ‘siseme sikukwambia, wajipalia makaa.
















       [ Imeandaliwa na: nyembo @ 5:30 AM ] [ ]



       Monday, January 23, 2006  

    LA KWANGU,LAKO LI-WAPI ?
    Ndugu yangu Bw. Boniphace Makene, aliandika shairi lake katika Blog yake BONYEZA HAPA akiuliza kama mimi ni malenga mbona sina jina. Ingawa niliwahi kuona kwanza maoni yake kupitia Blog ya Mshairi Mwenzetu Bw. Mkwinda, pale nakumbuka nilimjibu kwa ufupi kuwa jina langu ni Hud-hud.

    Lakini naona ipo sababu sasa ya kumjibu hapa kwa kuwa nae alichukua jukumu la kuniuliza swali hilohilo katika Blog yake eti jina langu nani?

    LA KWANGU, LAKO LI- WAPI?

    Si mwingine ni kijana, wa snowhite Bwana,
    Hud-hud naitwana, shairini kushindana,
    Sio kwamba najivuna, nina jina simtwana,
    La kwangu, lako liwapi,alo na lake nanene.

    Wataka kujua jina, lako mbona hujanena?
    pia wataka kutuna, na upele kunikuna!
    eti malenga wa jana, majina taka juana,
    La kwangu, lako liwapi,alo na lake nanene

    Mimi siwezi kukana, Malenga ninalo jina,
    Pengine mnaniguna, kwa mkao wa kigwene,
    Ushairi si dhumna, Mchezo wa shytwana,
    La kwangu, lako liwapi, alo na lake nanene.

    Kujifana kamishina,kuvizia kwenye kona,
    Ukapanga vyako vina, kuniuliza Nomina,
    Maswali yakakukwina, kizazicho sifiana,
    La kwangu, lako liwapi,alo na lake nanene.

    La kwangu, lako si jina, au jinalo wakana?
    Ama walificha sana, ni tusi utatukana?
    Napenda kukumbushana, nawe wangu swahibana,
    La kwangu, lako liwapi, alo na lake nanene.

    Mkwinda lake janena, lipi mtaambiana?
    Na vipi mtaitana, majina kwa kutajana?
    Hud-hud lapangana,herufize rudiana,
    La kwangu, lako liwapi,alo na lake nanene.

    Mbona wataka kwazana, kwa maneno kurushana?
    Mimi tabu wala sina, sipendi kuzinguana,
    Mwapenda sana vutana, kwa kujifana mabwana.
    La kwangu, lako liwapi, alo na lake nanene.

    Wangu ‘koo natokana, babu yangu ni Kamana,
    Baba yangu Saadana, mtunzi wa kale sana,
    Ujiji ni yangu jannah, tipuzi ya langu shina.
    La kwangu, lako liwapi, alo na lake nanene.

    Nane beti tulizana, ili tupate juana,
    Nami nasaili tena, ni vipi tutakwitana,
    Na wengine kutajana, ili mpateitwana,
    La kwangu, lako li wapi, alo na lake nanene

       [ Imeandaliwa na: nyembo @ 10:17 PM ] [ ]


     

    Bwana mkwinda aliandika, Utungo wake mzuri haswa kuhusu suala la Ukimwi lililoitwa (SILO N’LILO),walakini si kwamba sikubali alichotunga, bali ni vema tukubaliane kuwa jamii imeingia katika hali ngumu ya kulidhibiti suala hili, watu wa dini wakiseama ni baa, janga toka kwa Mungu, kutokana na maasi na tabia zisizo njema tulizonazo, huku watu wafya wakisema muda waenda matiti, Ukimwi si janga wala baa toka kwa Mungu ni ukosefu wa kinga mwilini kutokakana na mashambulizi ya kirusi cha HIV.
    Katika utata huo kila mmoja anaona ana jukumu la kupambana kutokomeza ama janga au ugonjwa huo, lakini kila upande ukiulaumu mwingine kuhusu uzuiaji wa Mipira kondomu au uruhusuji wa mipira hiyo, kwangu hiki ni kitendawili, nasema Ukimwi ni janga au Ugonjwa?

    HIVI UKIMWI NI NINI?

    Hivi Ukimwi nini, ni ugonjwa au baa?
    Malenga wa bloguni, mimi napigwa butwaa,
    Naomba nsaidieni, nimebaki naduwaa,
    Mwenzenu naelemewa, si dhihaka nawambia.

    Mungu kwa nini idhini, kama Ukimwi ni baa?
    Watu ingia penzini, na tunda kujitwalia,
    Maneno ya chichini, kidume kutongozea,
    Mwenzenu naelemewa, si dhihaka nawambia.

    Mtoto vipi kosani, kama Ukimwi ni baa?
    Bado hajenda jandoni, mbona umemfikia?
    Vipi ataweza zini, ama ngono kutendea?
    Mwenzenu naelemewa, si dhihaka nawambia.

    Vipi ataweza zini, hajui kamwe kutenda?
    Na wala si mwanajini, kila kitu kukijua,
    mbona sipati yakini, chanzoche yeye ugua,
    Mwenzenu naelemewa, si dhihaka nawambia.

    Mke aliye ndoani, iweje akaugua?
    Mumewe amwamini, tunda peke kumpea,
    Tena chumbani sirini, wenyewe wafurahia,
    Mwenzenu naelemewa, si dhihaka nawambia.

    Mme aliye makini, virusi vimemjaa,
    Ashinda Msikitini, swala tano kuswalia,
    Jumapili kanisani, Misa hutuongezea
    Mwenzenu naelemewa, si dhihaka nawambia.

    Mshauri namba wani, sote twamtegemea,
    Nembo mpaka chupini, uzinzi kukatazia,
    Kaupata si utani, wapi najiulizia
    Mwenzenu naelemewa, si dhihaka nawambia.

    Wapi ameutoani, bado napata fadhaa,
    Mungu katubaguani, ili tupate jikwaa?
    Haukuwepo zamani, katika hii Dunia,
    Mwenzenu naelemewa,si dhihaka nawambia.

    Sasa naomba jibuni, mtego kuutegua,
    Bado nipo mashakani,msiwate n’elezea,
    Sasa nipo subirani, majibu kuyangojea,
    Mwenzenu naelemewa, si dhihaka nawambia.

       [ Imeandaliwa na: nyembo @ 7:19 AM ] [ ]



       Wednesday, January 18, 2006  

    SITAWATA KUANDIKA MWANDIKO TABADILI!

    Kwa jina lake rasul, nataka toa kauli,
    Jalia katakabali, zangu dua kukubali,
    sijui kazinakili, hasirazo kuzikili?
    Sitawata kuandika, mwandiko tabadili.

    Mwandiko tabadili, nipate kutakabari,
    kauli zilo kalili, zisiwe zangu johari,
    ili zisitashifili, ziwe zenye ikisiri,
    Sitawata kuandika, muandiko tabadili.

    Tungo sintozibadili, kwa kuwa ni tabasuri,
    kanijalia jalali, kutunga kwa tafakuri,
    kuacha kwangu muhali, wala sina stighari,
    Sitawata kuandika, muandiko tabadili.

    Utunzi wako mkali, nanena kwa udhahiri,
    Makene amekubali, Ndesanjo amefasiri,
    Mwandani ameujali, nami naona U-duri
    Sitawata kuandika, mwandiko tabadili.

    Ni wako wewe fahali, mwenye tungo zidururi,
    Mkwnda u mfadhili, kwa tungo zenye fahari,
    tungoze nazifaili, na pia nazifahiri,
    Sitawata kuandika, mwandiko tabadili.

    Kalamu yangu fasili, kamwe haina jeuri,
    tena siyo ya fedhuli, hii haina firari,
    naiacha filhali, ili nisije kithiri,
    Sitawata kuandika, mwandiko tabadili.

       [ Imeandaliwa na: nyembo @ 2:15 AM ] [ ]



       Monday, January 16, 2006  

    NO FEAR FOR THE FUTURE !

    KUNENA KANA KWANUKA,NIKUKOME KUKUNENA!

    Nasaha kwa rafikana, rafiki twaandikana,
    kunasihi kazi sana, ingawa wapuuzana,
    pengine utaikana, nasaha kudurusana,
    Kunena kana kwanuka, nikukome kukunena.

    Nalisoma yako jana, jana ibakile jina,
    hakika ulitukana, kuniona kinda sana,
    hayarudishiki tena, yaliyokwenda na jana,
    Kunena kana kwanuka, nikukome kukunena.

    Mkwinda ulitukana, Makene kacheka sana,
    Mwandani kanyamazana, mawazo yakajazana,
    kwa tungo zilopangana, shime nandika tena,
    Kunena kana kwanuka, nikukome kukunena.

    Kana kwanuka kunena, nikukome kukunena,
    kwa makonzi kutwangana, ni nje ya malengana,
    nini kitakufaana, kumpiga muungwana,
    Kunena kana kwanuka, nikukome kukunena.

    Beti sasa zapangana, kipigo kukikwepana,
    sanjarina naombana, hasirazo punguzana,
    wewe mwanafasihana, makini kumakiana,
    Kunena kana kwanuka nikukome kukunena.

    Naomba sasa patana, kwa jinale subhana,
    mbona umeparamana, kana toto la shetana?
    toka zako ten tana, kabliya siku jana
    Kunena kana kwanuka, nikukome kukunena.

    Kosa langu lipi sana, nakuuliza kijana!
    fananisho langu fana, la mauti mautana?
    au tatari tatana, tungo iloshindikana?
    Kunena kana kwanuka, nikukome kukunena.

    Au tatari tatana, swahiba twaulizana,
    chanzo hasira jazana, na sura kuvimbiana?
    mchuzi mchachu sana, nani ameuchachana?
    Kunena kana kwanuka nikukome kukunena.

    Kunena kana kwanuka, nikukome kukunena,
    kufuli fungo fungana, la Abdilatif bwana,
    heshima kwa mkwasana,tungoze zaongozana,
    Kunena kana kwanuka, nikukome kukunena.

    Kalamu naiachana, tena nakuomba sana,
    malenga kushikamana, na sio kutukanana,
    sifa yetu kushindana, tungo kupandishiana,
    Kunena kana kwanuka, nikukome kukunena.

    Nawaomba radhi sana wasomaji kwa kazi hiyo hapo juu, natumai hamkuzoea kuona tungo za aina yoyote zinazokwenda kwa vina na mizani, nimelazimika kuandika tungo hiyo kwa kuwa mwanabaraza mmoja Bw. Mkwinda ambaye ni rafiki yangu, alipoandika shairi lake katika Blog yake aliloliita kwa jina la Fasihi tata, bonyeza hapa kuona kazi yake hiyo, niliamua kuweka maoni yangu baada ya kumuona Malenga mmoja na mwanabaraza pia anaitwa Mwandani keshatoa maoni yake kiushairi pale chini.

    Kwa hakika aliyajibu maoni yangu kwa tungo zilosimama kwa Shairi aliloliita Chachandu za Uchachizi, baada hapo Mshairi na mwana baraza mwingine Boniphace Makene alitoa maoni yake akikataa kutumia mfumo wa ushairi na kunipa hamasa kuamua kumjibu kwa haraka kwa beti mbili za kishairi.

    Lakini niliazimu iwapo nikipata muda basi nitamjibu inavyostahili zaidi, hii ndio sababu ya tungo hiyo hapo.

       [ Imeandaliwa na: nyembo @ 5:27 AM ] [ ]


    :